News in KiSwahiliNews in KiSwahili

KONGAMANO LA UWEKEZAJI WA NCHI ZINAZOPAKANA NA ZIWA TANGANYIKA

View descriptionShare

Nchi zinazozunguka Ziwa Tanganyika pamoja na Rwanda leo zimehitimisha kongamano la kimataifa la uwekezaji na biashara katika ukanda huo ambalo limefanyika mjini Kigoma nchini Tanzania, huku likiamsha ari ya kufanya mageuzi katika mahusiano ya kiuchumi na utatuzi wa changamoto za kisera katika nchi za ukanda huo. Mwandishi wetu Prosper Kwigize ametuandalia ripoti ifuatayo kutoka Kigoma

Katika kongamano hilo ambalo linahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, taasisi na makampuni ya kibiashara, Mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini Tanzania na nje ya Tanzania na mamlaka za udhibiti kutoka nchi za Burundi, DRC, Rwanda, Tanzania na Zambia washiriki wamelalamikia kuwepo kwa vikwazo vingi vya uwekezaji hususani kwa nchi ya Tanzania ambayo ni lango kuu la biashara kwa nchi zisizokuwa na bahari. 

Malalamiko zaidi yametolewa kwa mamlaka ya bandari Tanzania, shirika la Reli, na mamlaka ya mapato, Mamlaka ya usafiri na usafirishaji majini na Idara ya uhamiaji kwa kutokuwa rafiki kwa wawekezaji wa nje na wa ndani kutokana na kuwepo kwa urasimu na mlolongo wa tozo, ucheleweshaji na uhamishaji wa mizigo katika bandari ya Dar es Salaam pamoja na mizengwe katika minzani ya kupima miziko wawapo njiani kuelekea katika nchi zao.

Bahigana Eulade ambaye ni mfanyabiashara mkubwa kutoka Rwanda ni miongoni mwa wageni walioilalamikia Tanzania katika mazingira ya biashara

Naye mfanyabiashara maarufu wa utalii na uwindajii wa wanyamapori nchini Tanzania Bw. Mohsin Shein licha ya kupongeza kuwepo kwa mageuzi kadhaa ya kimfumo lakini ameishauri serikali ya Tanzania kupunguza msululu wa mamlaka za udhibiti katika biashara  ili kuvutia wawekezaji wengi Zaidi kutoka ndani na nje

Viongozi wa mamlaka hizo wamekiri kuwepo na malalamiko na kwamba fursa ya majadiliano ipo wazi ili kuondoa vikwazo vya uwekezaji kwa nchi zote huku wito wa majadiliano ukitolewa kwa wadau, Mkurugenzi wa Shirika la wakala wa Meli Tanzania TASAC Bw. Kaimu Abdul Mkeyenge ni mmoja kati ya walioahidi kutatua changamoto kwa mujibu wa sheria.

Kongamano hilo la siku 3, limehitimishwa na Waziri wa Tawala za mikoa na serikali za mitaa nchini Tanzania Bw. Innocent Bashungwa kwa niaba ya waziri wa uwekezaji nchini Tanzania kwa kuweka bayana umhimu wa kila nchi kuweka mazingira Rafiki ya uwekezaji huku akipongeza uamuzi wa kuwepo kwa mijadala ya kiuchumi katika ukanda wa Ziwa Tanganyika.

Uimara wa uchumi, usalama na mahusiano ya kimataifa katika eneo la nchi za maziwa makuu hutegemea uimara wa mahusiano ya kiuchumi hususani usafiri na usafirishaji kupitia ziwa Tanganyika linalozifikia nchi 4 za SADC na Afrika Mashariki. 

  • Facebook
  • Twitter
  • WhatsApp
  • Email
  • Download

News in KiSwahili

A news and current affairs show produced live by the current affairs team.
Social links
Recent clips
Browse 1,121 clip(s)